Umoja wa Kiuchumi wa nchi za Eurasia, mhimili wake mkuu ukiwa ni Russia na kujumuisha nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Kazakhstan, Armenia, Belarus, na Kyrgyzstan, zenye eneo la zaidi ya kilomita za mraba milioni 20 (sawa na asilimia 15 ya eneo la ardhi la Dunia) na idadi ya watu zaidi ya milioni 182, ni mmoja wa washiriki muhimu zaidi wa kiuchumi katika eneo la Eurasia. Umoja huo una uwezo mkubwa wa kuzungusha mtaji, kubadlishana bidhaa na huduma; na unajulikana kama moja ya masoko yanayokua kwa fursa za uwekezaji duniani.
Mkataba wa biashara huria kati ya Iran na Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia ulitiwa saini Desemba 25, 2023 katika mji wa Saint Petersburg, Russia. Mkataba huo ulitiwa saini kwa lengo la kuwezesha mabadilishano ya kibiashara kwa kupunguza au kuondoa vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru na kupanua ushirikiano wa kiuchumi. Kufuatia kusainiwa makubaliano hayo, suala la kukuza uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia na maendeleo yao ulizingatiwa zaidi kuliko hapo awali, na sasa umeshuhudia ukuaji mkubwa. Kukuza mahusiano haya ni muhimu sana kwa pande zote mbili, sio tu kutokana na mtazamo wa kibiashara lakini pia kulingana na mtazamo wa kisiasa na wa kimkakati.
Nchi wanachama wa Eurasia
Kwa upande wa kiuchumi, kuimarishwa biashara kati ya Iran na nchi wanachama wa Eurasia ni fursa kwa pande mbili. Kwa upande mmoja, ushirikiano huu unapelekea kufikiwa masoko makubwa ya kimataifa ya bidhaa za Iran na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi wa Iran na mataifa yenye nguvu za kikanda kama vile Russia. Na katika upande mwingine, nchi wanachama wa Umoja wa Eurasia zinaweza pia kufaidika na eneo la kijiografia la Iran, miundombinu ya usafiri, na miundo mbinu na suhula wezeshi za usafirishaji. Wakati huo huo, Iran inaweza kutumika kama daraja la kuunganisha Mashariki na Magharibi na kuimarisha nafasi yake katika mnyororo wa ugavi wa kikanda.
Faida nyingine muhimu ya kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Iran na Eurasia ni kupiga hatua katika kuachana na matumizi ya sarafu ya dola katika biashara ya pande mbili. Katika miaka ya hivi karibuni, hatua ya Marekani ya kutumia vibaya dola kwa lengo la kutoa mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi kwa nchi zisizofungamana na siasa za Washington imepelekea nchi nyingi duniani kutaka kupunguza utegemezi wao kwa sarafu ya dola. Hatua hii ina umuhimu wa kistratejia hasa kwa nchi kama Iran na Russia ambazo zimelengwa moja kwa moja na vikwazo vya Marekani. Katika fremu hii, kuimarisha uhusiano na Umoja wa Kiuchumi wa Nchi za Eurasia, katika muda mrefu, inaweza kufungua njia ya utekelezaji wa sera ya kuachana na matumizi ya sarafu ya dola na kuwa huru kifedha mkabala wa mfumo wa fedha unaohodhiwa na Magharibi.
Eurasia na mkakati wa kuachana na matumizi ya sarafu ya dola
Katika muktadha huu, Iran na Russia zinaongeza matumizi ya sarafu za kitaifa za rial na ruble katika mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi mbili. Wakati huo huo mazungumzo pia yanaendelea kati ya wanachama wengine wa umoja huo ili kutumia sarafu za ndani. Sera hii inaweza kwa kiasi kikubwa kuzikomboa nchi wanachama wa Eurasia ili kujivua na udhibiti wa mifumo ya kifedha ya kimataifa, hasa mfumo wa dola. Wakati huo huo, kutumia sarafu mbadala, kubadilishana biashara na hata kufanyika malipo kwa kutumia sarafu za kidijitali ni masuluhisho yanayoweza kuharakisha mchakato wa kuachana na matumizi ya dola na hivyo kuandaa msingi wa ustawi endelevu zaidi wa kiuchumi.
Katika uga wa usalama pia, kuwa karibu Iran na nchi wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia kunaweza kutoa mchango chanya katika kuimarisha uthabiti na usalama wa kikanda. Kuhusiana na hili, mazungumzo ya karibuni kati ya Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia na viongozi wa Iran kuhusu muundo mpya wa usalama katika Eurasia kwa kuzishirikisha nchi na taasisi za kikanda, yanaonyesha hatua ya pamoja ya Tehran na Moscow kwa ajili ya kuasisi mifumo huru ya usalama, nje ya fremu za nchi za Magharibi.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa kukua kwa biashara kati ya Iran na Umoja wa Kiuchumi wa nchi za Eurasia, hususan kuongezeka kwa mauzo ya nje, ni hatua ya kwanza katika njia ya muda mrefu ya kuimarisha ushirikiano na nchi za Eurasia.
342/
Your Comment